Kahama. Mradi wa kufuga nguruwe uliokuwa ukitekelezwa na Kikundi cha Twaweza, Kata ya Mwendakulima, wilayani Kahama umefungwa baada ya fisi kuvamia zizi na kuwatafuna wote.
Akizungumza mjini hapa juzi, Meneja wa Shirika la Shdepha Kahama, Venance Mzuka alisema mradi huo ni kati ya mingine mitano inayotekelezwa kwenye kata hiyo.
Shirika hilo linasimamia vikundi 12 vya uzalishaji kwenye kata hiyo vinavyofadhiliwa na Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi.
Katika kikao cha wadau, Mzuka alisema ufugaji nguruwe ndiyo ulikuwa na soko la uhakika, lakini sasa umefungwa baada ya fisi kula mifugo hiyo.
Hata hivyo, Mzuka alisema miradi mingine ya ufugaji kuku, mbuzi, ng’ombe, kilimo na usindikaji mafuta ya kupakia unaendelea kwenye vikundi vinane kati ya 12 vilivyopo.
Mzuka alisema Mgodi wa Buzwagi unaomilikiwa na Kampuni ya African Barrick Gold Mines (ABG), umechangia Sh10 milioni huku vikundi nane vikipewa Sh6 milioni na zinazosalia zitagawiwa kwa vinne baada ya kukamilisha usajili.
Hata hivyo, wana kikundi hao walilalamikia ukosefu wa masoko ya kuuzia bidhaa zao, kwa madai ya kuwapo kwa gharama kubwa ya uendeshaji ikiwamo ununuzi wa vyakula vya mifugo. Kufuatia hali hiyo, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mji wa Kahama, Fanuel Reuben alisema ili kumaliza tatizo la masoko inatakiwa kuwa na kituo rasmi cha kuuzia kitakachokuwa mjini, wateja watawafuata moja kwa moja walipo na kununua bidhaa zao
0 comments :
Post a Comment