Ikulu imeeleza kuwa imeshindwa kutimiza ahadi yake kwa taifa ya kulipatia Katiba Mpya ifikapo Aprili 26, 2014.
Katibu Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue alilieleza gazeti hili kuwa kwa hali ya mchakato huo ilivyo sasa, wameshindwa kufikia lengo hilo, lakini hawajakata tamaa kuhusu kupatikana Katiba Mpya ndani ya mwaka huu.
“Kweli matarajio ya awali yalikuwa hayo, lakini kama unavyoona hali ilivyo, ni vigumu kusema matarajio mengine, ingawa majadiliano yaliyofanywa mwaka huu ni lazima Katiba inayopendekezwa iwasilishwe kwa wananchi na mwakani tutakuwa na Katiba Mpya,” alieleza Balozi Sefue.
Katika hali isiyoeleweka Balozi Sefue alisisitiza msimamo wa awali wa Serikali kwamba Katiba itakayopatikana itatumika kwenye Uchaguzi Mkuu, unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.
Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), Dk. Willbroad Slaa, alisema hilo ni fundisho kwa Serikali kwamba kiburi na jeuri havitakiwi katika masuala yanayohusu umma.
Alisema muda huo wa kupatikana Katiba Mpya ulipotangazwa, walioanzisha kilio cha kudai Katiba Mpya nchini ambao aliwataja kuwa ni vyama vya upinzani vya siasa, taasisi mbalimbali za kijamii walipinga na kutoa ushauri kwa Serikali, lakini walipuuzwa.
Dk. Slaa alisema walipendekeza kwamba badala ya kupeleka mchakato wa Katiba mchakamchaka, warekebishe kwa mara ya 15 Katiba inayotumika, ili iende na wakati wa sasa ikiwamo Uchaguzi Mkuu ujao kwa lengo la kutoa muda wa kutosha kwa mchakato wa taifa kupata Katiba Mpya.
“Lakini walitukebehi na kututukana sana, sasa kiko wapi Aprili 26 hiyo hapo na Katiba haijapatikana na kusema itapatikana mwaka huu na kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu mwakani ni ndoto za mchana,” alieleza Dk. Slaa.
Dk. Slaa alisema tukio hilo liwe fundisho kwa Serikali, wawe wakweli, wanyoofu na wafahamu kuwa nje ya Serikali kuna watu makini na wanaojua vilivyo mchakato wa Katiba.
Alisema ana taarifa za Bunge Maalumu kuahirishwa Mei 9, 2014 ili kupisha Bunge la Bajeti. Hivyo mategemeo ya Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao, yanatia shaka.
“Kwa akili ya kawaida tu isiyohitaji elimu ya chuo chochote, kutumia Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ni jambo lisilowezekana kwa hiyo waache kutuletea matumaini yasiyokuwapo, sisi siyo watoto wadogo,” alieleza Dk. Slaa. endeleaa
0 comments :
Post a Comment