Pata Habari Motomoto za Nje na Ndani ya Nchi kwa njia ya E-mail, Andika E-mail yako hapo chini.


Home » » Wasaka urais waibukia msibani, soma upate kuwafahamu

Wasaka urais waibukia msibani, soma upate kuwafahamu


Rais Kikwete akihani msiba wa Ng’hwani

LICHA ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutoa karipio kali kwa baadhi ya makada wake watano waliotuhumiwa kuanza kampeni za urais mapema, wagombea hao wameendelea kuchepuka karipio hilo, safari hii baadhi wakijipenyeza hadi msibani kuendeleza kwa siri harakati hizo.

Hali hiyo imejitokeza hivi karibuni kwenye mazishi ya aliyekuwa Mwenyekiti mstaafu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Shinyanga – SHIRECU na kada wa muda mrefu wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na baadaye CCM, Edward Masanja Ng’hwani.

Ng’hwani aliyefariki kwa ugonjwa wa kansa katika Hospitali ya Ocean Road, jijini Dar es Salaam, Aprili 13, na kuzikwa nyumbani kwake katika kijiji cha Bunamhala, nje kidogo ya mji wa Bariadi, Mkoa wa Simiyu, Aprili 18, mwaka huu.

Sekeseke hilo lilianza na Rais Jakaya Kikwete, aliyefuatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, kwenda kuhani kwa ndugu wa marehemu Ng’hwani maeneo ya Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam, Aprili 17, mwaka huu, ambako mwili wa marehemu ulilala kwa maandalizi ya kusafirishwa kwa ndege kwenda wilayani Bariadi kwa mazishi, ambapo Rais alitoa ndege ndogo ya Serikali kusafirisha mwili wa marehemu.

Katika mazishi hayo, CCM kiliwakilishwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira na kuhudhuriwa pia na maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Simiyu na mikoa jirani ya Mwanza, Geita na Shinyanga.

Katika salaamu zake za rambirambi, Wassira alimwelezea marehemu Ng’wani kuwa mwanachama shupavu wa CCM na mpatanishi aliyesimamia haki daima kwa kutetea wanyonge na wote wasio na sauti nchini.

Alisema, alimfahamu pia kama kiongozi makini wa vyama vya ushirika kwa sehemu kubwa ya maisha yake, mkulima stadi ambaye Wassira aliwahi kupewa na marehemu shamba kubwa la kulima mahindi miaka kadhaa iliyopita wakati mambo ya siasa yalipomwendea kombo.

Wassira alitoa ubani kwa familia ya marehemu kutoka CCM Makao Makuu Dodoma na ubani wake mwenyewe ambao kiasi wala thamani yake hakuitaja kwa madai kwamba huo haukuwa mchango wa harusi au “harambee” ya kukusanya fedha.

Katika hali iliyoashiria kuwapo kwa minyukano ya chini kwa chini ya kikampeni, safari ya Membe kwenda kuhani Kigamboni jijini Dar es Salaam, siku tatu kabla ya hapo ilionekana kuwazindua wagombea wengine watarajiwa wakajiona kuanza kutimuliwa vumbi.

January Makamba, mmoja wa wanaCCM walioitwa na kuhojiwa kisha kupewa karipio kali na Chama kwa kuanza kampeni mapema, aliwaambia waombolezaji kwamba alimpigia simu mjane wa marehemu Ng’hwani, mama Juliana Mahongo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bariadi, kumpa pole na kutoa udhuru wa kutohudhuria mazishi hayo, lakini baadaye alibadili nia ghafla na kuamua kuhudhuria mazishi hayo.

Nilimpigia simu mke wa marehemu Ng’hwani kumpa pole na kumweleza kwamba nisingehudhuria mazishi ya mumewe kutokana na kubanwa na majukumu mengine, lakini muda mfupi baadaye nafsi ilinisuta, nikaamua kuja”, alisema Makamba akionesha kwamba hakuwa katika msafara wa Wassira.

Alisema, alikuja kuwapa pole watani zake Wasukuma, lakini muda wote alipokuwapo hapo hakwisha kuchepuka pembeni mara kwa mara kwa mazungumzo “nyeti” na vijana wa UVCCM waliokuwa wakionana naye kwa makundi, kuashiria kwamba alikuwa kwenye “mawindo”.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja alitoa salaam za rambirambi za mkoa wake pamoja na salaamu na ubani kutoka kwa Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.

“Nimetumwa na Edward Lowassa, nifikishe salaam hizi pamoja na ubani kwa wafiwa kwa maelezo kwamba, Lowassa yupo pamoja nanyi katika msiba huu mkubwa kwa Wanasimiyu,”

“Lowassa ni mpenda watu; msiba huu umemgusa yeye na familia yake na anawaombea Mungu awatie nguvu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,” alisema Mgeja.

Haikufahamika ni kwa nini ujumbe wa Lowassa ulitolewa na Mgeja ingawa ni wazi kwamba Mgeja ni mpiga debe mkubwa wa Lowassa na wadadisi wa mambo ya siasa kuhusiana na mbio za urais mwaka 2015, wanaona kuwa Lowassa alituma salaamu hizo baada ya kuhisi “wapinzani” wenzake watajiimarisha msibani.

Mikoa ya Kanda ya Ziwa, ukiwamo Mkoa wa Simiyu, ni mtaji mkubwa kwa wanasiasa nyakati za uchaguzi ambapo msafara wa wajumbe kwenda kwenye mikutano ya uchaguzi umepewa jina “treni ya ushindi”.

Kuhudhuriwa kwa mazishi ya Edward Ng’hwani na vigogo wawili hao wa CCM na mwakilishi mmoja wa wagombea urais watarajiwa ambao kwa maudhui yote walionekana kuhudhuria kwa juhudi binafsi, kumetafsiriwa kwa usahihi kuwa ni moja ya mbinu za kuanza kuisaka mapema treni hiyo ya ushindi, licha ya karipio la Chama.

Marehemu Edward Masanja Ng’hwani alizaliwa mwaka 1935 wilayani Bariadi. Katika uhai wake, ametumikia sekta ya ushirika kuanzia na ngazi ya Katibu wa Ushirika, Mwenyekiti wa SHIRECU na amewahi pia kuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika nchini (CUT).

Kisiasa amewahi kuwa Mbunge wa Bariadi mwaka 1975 hadi 1980, Kamanda wa Vijana na Mweka Hazina wa CCM, Mkoa wa Shinyanga. Ameacha wajane sita, watoto 39 na vitukuu 15.

Vigogo wa CCM walioitwa na kuhojiwa na hatimaye kupewa karipio kwa kuanza kampeni za urais mapema kwa hatari ya kukigawa chama hicho ni Edward Ngoyayi Lowassa, Bernard Membe, Steven Wassira, January Makamba, Frederick Sumaye na William Ngeleja. Kwa hukumu hiyo pia, Chama kiliwapiga marufuku pamoja na wapambe wao, kufanya kampeni kwa miezi 12 hadi Februari mwakani.chanzo raia mwema

0 comments :

Post a Comment

 

Copyright © 2013. THE WORLD OF TODAY - Haki zote zimehifadhiwa
Template Modify by World of Today TEAM
Proudly powered by Blogger