Dar na Iringa. Baraza la Maaskofu la Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), limewataka wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kurudi bungeni bila masharti na kuendelea na mjadala wa Katiba kwa manufaa ya taifa.
Pia, Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Jimbo la Mashariki Kaskazini, Geoffrey Massawe amewaomba wajumbe wa Bunge la Katiba kuungana na kuwa kitu kimoja katika mchakato wa kujadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba.
Kauli hizo za maaskofu hao zimekuja siku moja baada ya ile ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kusema kuwa hatima ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu utategemea Ukawa, kurejea katika Bunge Maalumu kuipitisha Katiba Mpya kwa wakati.
Askofu Massawe alitoa ombi hilo wakati wa ibada maalumu ya sherehe ya maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo nchini iliyofanyika katika Kanisa la TAG Kinondoni, Dar es Salaam.
Akitoa salamu za TEC wakati wa kuadhimisha miaka 25 ya uaskofu ya Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa kwenye Uwanja wa Kichangani, Iringa, Makamu Rais wa TEC, Mhashamu Severine Niwemugizi alisema ni vyema wajumbe hao wakarudi kwenye Bunge hilo linalotarajia kuanza Agosti 5, mwaka huu.
“Ninatumia neno kuwataka na siyo kuwaomba warejee bungeni mwezi ujao. Wasipofanya hivyo au kufanya mizengwe mingine na kutupatia Katiba isiyotufaa, nitawaomba Watanzania wote tuweke uzalendo mbele na kuikataa Rasimu ya Katiba itakayoletwa pia tuwanyime uongozi katika Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema.
Alisema wameshuhudia mambo ya aibu katika Bunge la Katiba kabla ya kupisha Bunge la Bajeti na maoni ya wananchi yaliyokusanywa kupitia tume halali yakibezwa.
Alisema tume ile iliongozwa na wazee wenye uzoefu mkubwa waliolitumikia taifa kwa muda mrefu na kutumia fedha nyingi za walipa kodi lakini yalipuuzwa jambo ambalo siyo sahihi.
“Nchi imepoteza dira, wananchi wako njiapanda hawajui kama watapata Katiba au la na ubinafsi umechukua nafasi kuliko uzalendo kwa taifa,” alisema.
Niwemugizi aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika kuboresha Daftari la Wapigakura na kujitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu na ule mkuu utakaofanyika mwakani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu, Pinda aliwataka viongozi wa dini kuliombea taifa kuwa na amani kutokana na matukio makubwa ya Uchaguzi Mkuu na Katiba yaliyopo. Pinda alisema amesikia ujumbe uliotolewa na Askofu Niwemugizi na kuwa kiongozi makini ni yule anayekubali kukosolewa na kufanya marekebisho chanzomwanainch
0 comments :
Post a Comment