Pata Habari Motomoto za Nje na Ndani ya Nchi kwa njia ya E-mail, Andika E-mail yako hapo chini.


Home » » siri yawekwaa wazi: Serikali mbili ni maagizo ya JK, yamewekwa wazi na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi.

siri yawekwaa wazi: Serikali mbili ni maagizo ya JK, yamewekwa wazi na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi.



Mbeya. Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi amefichua sababu za chama hicho kushikilia msimamo wa muundo wa serikali mbili katika mjadala wa Katiba Mpya, akisema ni “maagizo ya mwenyekiti wa CCM”.


Mjadala wa Katiba Mpya ulikumbwa na mtikisiko baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza kitu alichokiita maoni yake binafsi wakati akizindua Bunge la Katiba kwa kueleza kuwa angependa muundo wa Muungano wa serikali mbili tofauti na Rasimu ya Katiba iliyopendekeza serikali tatu.


Mjadala huo ulivurugika kabisa baada ya kundi la wajumbe kutoka vyama vya upinzani waliounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia vikao likidai mjadala umepoteza mwelekeo kwa kuweka kando maoni ya wananchi ya kutaka muundo wa serikali tatu.


Akifungua mkutano wa Baraza la Utendaji la Umoja wa Vijana wa CCM wa Mkoa wa Mbeya juzi jioni, Zambi alisema mwenyekiti wa CCM alishawaambia kwamba msimamo wa chama ni kuhakikisha zinabaki serikali mbili kwenye Katiba Mpya.


‘’Vijana sasa lazima niwaeleze ukweli kuhusu muundo wa serikali, ni kwamba piga ua, CCM inataka kuimarisha muundo wa serikali mbili na hili ni agizo la mwenyekiti wetu Rais Jakaya Kikwete,” alisema huku akishangiliwa.


Alisema suala la Muungano ni maelewano na kwamba baadhi ya shughuli muhimu za Zanzibar zimehamishiwa Bara wakati nyingine za Bara zimehamishiwa Zanzibar.


Hata hivyo, alisema kero iliyopo kwa sasa kwenye Muungano huo ni namna ya kugawana mapato makubwa ambayo alisema Serikali inaendelea kuyafanyia kazi.


“Rais Kikwete katika kutueleza msimamo wa chama, pia alifafanua vizuri suala la serikali tatu kuongeza gharama za uendeshaji, jambo ambalo hata mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba aliliona, ingawa alifafanua kwamba halina namna,” alisema.


Zambi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, alisema anamshangaa Mwenyekiti wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe anapotamka kwamba serikali tatu ni lazima.


“Vijana wote na wanaCCM mkoani Mbeya naomba muelewe kwamba sisi chini ya mwenyekiti wetu wa CCM, Rais Kikwete, tumeamua muundo wa serikali mbili tu,” alisema.


Alisisitiza kwamba kama wachache hawataafiki msimamo huo kwa busara, Serikali ya CCM itaendelea na katiba iliyopo.


Akieleza sababu za msimamo wake wa serikali mbili wakati akizindua Bunge la Katiba, Rais Kikwete alizungumzia gharama za uendeshaji wa serikali tatu akisema katika muundo wa serikali tatu, Serikali ya Muungano haitakuwa na vyanzo vya uhakika vya fedha na kwamba hilo linaweza kusababisha kushindwa kulipa mishahara kama ya wanajeshi na hivyo kusababisha chombo hicho cha dola kuchukua serikali.chanzo mwananchi

0 comments :

Post a Comment

 

Copyright © 2013. THE WORLD OF TODAY - Haki zote zimehifadhiwa
Template Modify by World of Today TEAM
Proudly powered by Blogger