KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade,
amesema hatishwi na kauli ya mmliki wa Kampuni ya kufua umeme ya IPTL,
Herbinder Singh Seth ya kutaka akamatwe na kufikishwa mahakamani.
Kauli ya Kamishina Bade, imekuja siku chache baada ya Kampuni ya Pan
Africa Power Solutions (PAP) na IPTL, kuitaka Bodi ya Rufaa ya Kodi
nchini iamuru Kamishna Mkuu wa TRA, akamatwe na kupelekwa mahakamani kwa
hatua yake ya kufuta hati za kuthibitisha ulipaji wa kodi wa kampuni
hiyo katika ununuzi wa hisa za IPTL.
Akizungumza na MTANZANIA jijini Arusha jana, Bade alisema siku zote mamlaka yake haimwonei mtu juu ya ulipaji wa kodi.
“Sitishwi na mtu, tunatakeleza majukumu yatu kwa mujibu wa sheria
zilizopo. Kama ni Singasinga unayemsemea mimi simjui una maanisha nani?
Kama ni yule wa IPTL najua ni mlipa kodi wangu, lazima alipe tu,”
alisema Bade.
Alipoulizwa juu ya kauli ya Herbinder ya kutaka ashitakiwe mahakamani, Kamishna Bade alisema kauli hiyo hajaisikia.
“Hii kauli sijaisikia lakini kama ni kushitakiwa mimi nashitakiwa na
kupelekwa mahakamani kila siku. Hapa suala ni moja tu lazima kodi
ilipwe.
“Mlipa kodi ambaye nimemwambia alipe kodi lazima alipe, hatuna mzaha
katika kazi za taifa. Narudia na kusisitiza kauli yangu, hata huyu
mfanyabiashara unayemsema lazima alipe kodi haina mjadala, kama nimesema
alipe basi atalipa.
“Kama watu hawatalipa kodi basi sisi tutatumia mamlaka yote tuliyopewa kisheria kukusanya kodi husika,” alisema Bade.
Akizungumzia ushindi ilioupata TRA katika shindano la ulinganishi wa
taarifa za fedha, Kamishna Bade alisema ni mafanikio makubwa ambayo
yanapaswa kuendelezwa.
“Siku zote taaluma ya uhasibu huleta maadili kwa taifa nawahimiza wahasibu na wakaguzi nchini kutanguliza maadili,”alisema Bade.
Hatua ya TRA kufuta hati hizo, ilitokana na udanganyifu uliofanywa na
PAP kwa kuwasilisha nyaraka za kughushi za ununuzi wa hisa, hali
iliyoiwezesha kukwepa kodi ya Sh bilioni 8.68.
“Tunaomba bodi imwamuru Kamishna Mkuu wa TRA kutekeleza amri
iliyotolewa, pia bodi itoe amri ya kuondoa barua ya kamishna ya Novemba
27, mwaka huu ambayo ilifuta hati za kodi mpaka maombi ya msingi
yatakaposikilizwa,” inadai hati hiyo ya maombi.
Awali Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima akifunga mkutano huo,
alionyesha kusikitishwa na uchache wa wizara, taasisi za Serikali na
halmashauri katika shindano la ulinganishi wa taarifa za fedha.
“Bodi ya Uhasibu (NBAA) wamefanya jambo jema kulinganisha taarifa za
fedha. Hii inatupa utaratibu wa kuangalia wapi tumefanya vizuri na wapi
tunatakiwa kuboresha.
“Kisheria NBAA si chombo kinachopelekewa hesabu kwa ajili ya
kuzidhibitisha, isipokuwa nyinyi wenye fani mkitaka mjilinganishe mpo
vizuri?
“Nadhani tutahimizana japo si jambo la lazima ni la hiari. Lakini ni jambo zuri kushindana kujua ubora wa hesabu zenu.
“Katika kundi la taasisi za Serikali nitawaomba NBAA watuandikie
Wizara ya Fedha nasi tutamshauri waziri aandike barua kwa taasisi zote
kusisitiza uzuri wa jambo hili.
MADAI YA IPTL
Katika madai yake, IPTL ilisema hati hizo za PAP zilizofutwa ni zile
zenye namba 0049656 na 0049657 ambazo zilitolewa kwa ajili ya uuzaji
wa hisa kutoka Kampuni ya Mechmar na Piper Links Investment na kati ya
Piper Links na PAP.
Katika hati ya kiapo, Chandrasakaran alidai Desemba 23 mwaka jana
wadai walipata hati hizo za kuthibitisha walilipa kodi kwa ajili ya
uuzwaji wa hisa hizo.
Alidai Novemba 19, walalamikiwa walitoa taarifa ya siku sita kwa
BRELA wakionyesha nia ya kuziondoa hati hizo kwa mazingira kwamba
walalamikaji walipata mkataba feki wa mauzo ya hisa hizo.
“Kamishna si tu anabanwa na mamlaka, pia anatakiwa kufuata sheria za
nchi zikiwamo za bodi, kwa kukiuka amri anapoteza sifa za kuendelea
kushikilia nyadhifa hiyo aliyonayo,” alidai Chandrasakaran katika hati
ya kiapo.
Hata hivyo, kutokana na maombi hayo kuwasilishwa chini ya hati ya
dharura, bodi hiyo mbele ya Katibu wake, Respicius Mwijage iliamuru
yasikilizwe.
PAP na IPTL waliwasilisha rufaa pamoja na maombi ya zuio la muda
ambapo Novemba 26, Katibu wa bodi hiyo, Mwijage, alitoa zuio la muda kwa
Kamishna Mkuu wa TRA na Msajili wa Makampuni nchini (Brela) kuziondoa
hati hizo na kuacha hali ilivyo sasa iendelee kuwa hivyo.
Pamoja na kutolewa kwa amri hiyo, Novemba 28 TRA waliandika barua wakionyesha walishaziondoa hati hizo.
Zitto
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za serikali (PAC), Zitto
Kabwe, alisema kitendo kinachofanywa na mmiliki wa kampuni hiyo ni
kuonyesha jeuri ya fedha na kuidharau Serikali.
“Ana kiburi cha kifisadi na ni dalili za kuidharua Serikali, jambo
kama hilo linaweza kufanywa Tanzania tu, Serikali idhibiti dhihaka hii
kwa kuchukua hatua dhidi ya mtu huyu,” alisema Zitto.
Azimio la kwanza la Bunge juu ya kashfa hii, lilitaka Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), jeshi la polisi na vyombo
vingine husika vya ulinzi na usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu
wa sheria za nchi, dhidi ya Singh Seth ambaye ni mmiliki wa Kampuni PAP
na wengine wote waliotajwa na taarifa maalumu ya Kamati, kuhusika na
vitendo vyote vya kijinai kuhusu miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu
wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea.
MWIGULU: KODI LAZIMA ILIPWE
Akizungumza bungeni wakati wa kujadili ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), juu ya ukaguzi wa akaunti ya Tegeta
Escrow, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema lazima kodi ya
Serikali iliyokwepwa ilipwe.
Alisema kutokana na kutolipwa kwa kodi ya ongezeko la thamani, TRA
ilikuwa ikose Sh bilioni 26.97 lakini baada ya kubaini imeanza
kufuatilia na Sh bilioni 4 tayari zimelipwa.
“Niwahakikishie Watanzania kuwa kodi hii italipwa, hatuwezi kuacha kodi kwa tajiri,” alisema.
RIPOTI TA CAG NA KODI ILIYOKWEPWA
Kwa mujibu wa ripoti ya PAC, Septemba 9, 2012 Kampuni ya Mechmar
iliuza hisa saba kwa Piper Links ilizokuwa inamiliki katika Kampuni ya
IPTL kwa bei ya dola za Marekani milioni 6.
Hata hivyo, taarifa zilizowasilishwa TRA kwa ajili ya kukokotoa kiasi
cha kodi ya ongezeko la mtaji ambacho Mechmar ilitakiwa kulipa,
zinaonyesha hisa hizo zimeuzwa kwa Sh milioni 6 za Kitanzania badala ya
dola za Marekani.
Kutokana na udanganyifu huo, kodi ya ongezeko la mtaji iliyolipwa ni Sh 596,500, badala ya Sh 1,919,988,800 iliyopaswa kulipwa.
Inasema hisa hizo kutoka Kampuni ya Piper Links kwenda PAP, ziliuzwa
kwa gharama ya dola za Marekekani milioni 20, lakini taarifa
zilizopelekwa TRA zilionyesha zimeuzwa kwa dola za Marekani 300,000.
“Kwa mantiki hiyo taarifa ya CAG inaonyesha Piper Links ilitozwa na
kulipa kodi ya ongezeko la mtaji Sh 47,940,000 na Sh 4,800,000 kama
ushuru wa stempu (stamp duty),” ilisema taarifa hiyo.
Katika mahojiano, Kamishna Mkuu wa TRA aliifahamisha PAC kuwa kwa
gharama ya dola za Marekani milioni 20, kiasi cha kodi ya ongezeko la
mtaji kilichotakiwa kulipwa ni Sh 6,399,977,600 na si Sh 47,988,800, na
kwa upande wa ushuru wa stempu kiasi kilichotakiwa kulipwa ni Sh
320,000,000 na si Sh 4,800,000 Mtanzania
0 comments :
Post a Comment