Pata Habari Motomoto za Nje na Ndani ya Nchi kwa njia ya E-mail, Andika E-mail yako hapo chini.


Home » » Dk Mwakyembe aanza fagiafagia TRL

Dk Mwakyembe aanza fagiafagia TRL



Dar es Salaam. Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe ameagiza kung’olewa kwa baadhi ya vigogo wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ambao wanatuhumiwa kuhusika katika mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya kusafirisha kokoto kutoka India, ambayo yalibainika kuwa mabovu.


Mabehewa hayo ni kati ya 25 aina ya Ballist Hopper Bogie (BHB) yaliyoingizwa nchini Julai 24 yakiwa yamegharimu kiasi cha Sh4 bilioni na 20 yalibainika kuwa ni mabovu na kulazimika kuanza kutengenezwa kwa kificho.


Mkataba wa kununua mabehewa hayo ulisainiwa Machi 21, 2013 kati ya TRL na Kampuni ya Hindusthan Engineering and Industries ya India.


Jana, Dk Mwakyembe aliiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya TRL kuwasimamisha kazi mara moja kupisha uchunguzi, wahandisi wote waliokwenda India kwa ajili ya kufanya uhakiki wa ubora wa mabehewa hayo.


Alitoa maagizo hayo mbele ya Menejimenti ya TRL na wafanyakazi wa kampuni hiyo, katika kikao cha kuhitimisha mchakato wa kushughulikia malalamiko ya watumishi ambao wamekuwa wakidai malipo ya kima cha chini cha mshahara cha Sh300,000.


“Natoa siku 10 Bodi ya Wakurugenzi iwe imenipa majibu ya mchakato mzima wa ununuzi wa mabehewa 25 ya kokoto ulivyofanywa. Nataka uchunguzi ufanyike lakini wale wote waliokwenda India mara mbili kwa ajili ya kuthibitisha ubora wa mabehewa hayo wasimamishwe kazi mpaka taarifa za wasio na hatia zitakapobainika,” alisema.


Aliagiza kusimamishwa kazi kwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TRL na kuondolewa katika nafasi yake, mkuu wa idara ya fedha pamoja na kuvunjwa kwa bodi ya zabuni ya kampuni hiyo na kusitishwa kwa mikataba yote iliyopo kati kampuni hiyo na wazabuni.


Mikataba aliyoagiza kusitishwa ni pamoja na ule wa TRL na Kampuni ya Transroads inayoshughulikia upakiaji wa mizigo na kampuni ya R&A inayotekeleza ukarabati wa reli pamoja na urekebishaji wa mfumo wa mawasiliano huku akitaka kuondolewa kwa mzabuni anayehudumu katika Shule ya Msingi Itigi.


“Nataka bodi iende Itigi na iniambie imemchukulia hatua gani msimamizi wa mradi huu ambao mkataba wake unaonyesha kuwa chakula kinatolewa shuleni hapo lakini si kweli. Huwa naongea nikiwa natabasamu lakini ikibidi nitaiondoa bodi hii. Kuna Watanzania wengi wanaweza kufanya kazi hii, kama kuna mtu anaona hawezi basi aache mara moja.”


Alisema ripoti aliyonayo inaonyesha kuwa kati ya vitanda 320 vinavyoelezwa kuwapo katika shule hiyo, 260 ni vibovu huku magodoro yakiwa hayafai kwa matumizi ya binadamu.


Mgomo


Wafanyakazi wa TRL chini ya chama chao (Trawu) walianza mgomo wa kutaka majibu juu ya ongezeko la mishahara yao pamoja na malipo ya malimbikizo ya kati ya Julai na Oktoba mwaka huu na baada ya kutoelewana na uongozi, walilifikisha suala hilo wizarani.  mwananchi

0 comments :

Post a Comment

 

Copyright © 2013. THE WORLD OF TODAY - Haki zote zimehifadhiwa
Template Modify by World of Today TEAM
Proudly powered by Blogger