Pata Habari Motomoto za Nje na Ndani ya Nchi kwa njia ya E-mail, Andika E-mail yako hapo chini.


Home » » KAMA WEWE NI KIJANA AMBAYE UMEMALIZA CHUO NA BADO UNATAFUTA AJIRA, UBU SOMA UJUMBE HUU

KAMA WEWE NI KIJANA AMBAYE UMEMALIZA CHUO NA BADO UNATAFUTA AJIRA, UBU SOMA UJUMBE HUU


WASOMI WASIPOKUWA CHACHU YA MABADILIKO WASIMLAUMU YEYOTE.
Na Malisa GJ.
Jana nilitumiwa picha hii ikiwa na maelezo "Interview TRA Diamond Jubilee. Kila aliyepo kazini aiheshimu kazi"
Nilipouliza nikaambiwa ni interview ya mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) iliyofanyika ukumbi wa Diamond Jubilee. Kwa mujibu wa mtoa taarifa ambaye nae alikua sehemu ya wasailiwa; anasema jumla ya watu 23,653 walishiriki Interview hiyo na yeye namba yake ilikua 15,631.
Nilipouliza idadi ya waliohitajika kwenye kazi nikaambiwa ni watu 40 tu.. Nikachoka mwili na roho.! Unataka watu 40 halafu unafanya usaili wa watu 23,000? Huu ni zaidi ya UHUNI.
Watu 40 wanaohitajika kuajiriwa ni sawa na 0.16% ya watu 23,653 walioshiriki Usaili. Hii ni sawa na kusema katika kila watu 591 alihitajika mmoja tu. Kwa vyovyote vile usaili huu hauwezi kuwa wa haki maana ni ngumu sana kumpata mtu mmoja "potential" kati ya watu 591.
Hivi anayefanya usaili atatumia kigezo gani kumpata huyo mmoja miongoni mwa 591?? Umahiri wa lugha? Uwezo wa kujieleza? Uzoefu kazini? Ufaulu mzuri darasani? au muonekano?
Ikiwa watu wote 23,653 watafanyiwa usaili mmoja mmoja. Na angalau kila mmoja akapewa dakika moja tu ya kujieleza, watatumia jumla ya dakika 23,653 ambazo ni sawa na masaa 394.9 ambayo ni sawa na siku 16.
Hii ina maana kuwa wasailiwa hawakupata nafasi ya kujieleza; maana ili wajieleze angalau kwa dakika moja walihitaji siku 16, lakini usaili umefanyika siku moja. Hivyo Haihitaji miujiza kujua hata uwe "compitent" kiasi gani huwezi kupita kwenye usaili huu. Maana ni ngumu kuonesha "competence" yako kwenye mazingira kama haya.
Kwa lugha rahisi ni kuwa usaili huu ulikuwa ni "danganya toto" ya kumfanya kila aliyetuma maombi aridhike na kuona maombi yake hayakutupwa. Ni muendelezo wa serikali kuwatukana wasomi Tanzania.
Lakini wakati nikistaajabu hayo nikaambiwa NSSF nao walikua na usaili jana hiyohiyo. Na jumla ya walioitwa kwenye usaili huo ni takribani watu 8,000 licha ya kuwa waliokua wakihitajika hawazidi 50.
Matukio haya mawili yanatokea wakati ingali kwenye kumbukumbu juu ya usaili uliotia fora wa idara ya UHAMIAJI ambapo watu wapatao 11,000 walifanyiwa interview uwanja wa taifa ili kupata watu 70 tu.
Tukio lile lilionekana ni la kipekee kuwahi kutokea Afrika Mashariki na Kati, lakini hili la TRA limevunja rekodi. Vijana wanasema "hii ni funga mwaka". Kuita kwenye usaili watu 23,000 wakati unahitaji kuajiri watu 40 tu ni tukio la kihistoria kuwahi kutokea Kusini mwa Jangwa la Saharah tangu enzi za Pontio Pilato.
Lakini matukio haya yote ya watu kulundikana kwenye Usaili yanaashiria kitu kimoja kuwa TATIZO LA AJIRA NI KUBWA kuliko inavyodhaniwa. Kwa lugha rahisi issue ya ajira si tatizo tena ni JANGA LA KITAFA kama ilivyo njaa, mafuriko, Ukimwi, Ebola.!
Ni tatizo sugu ambalo serikali ya CCM imeonesha wazi kuwa imeshindwa kulitatua, na haina mpango wa kulitatua.
Nani atatue tatizo la ajira nchini? Viongozi wenye dhamana kila mmoja yuko busy na mambo yake.. Hata muitwe kwenye interview watu laki moja wenyewe haiwapi "pressure" maana wana uhakika watoto wao wataajiriwa tu tena kwenye mashirika makubwa au kama ni serikalini basi nafasi kubwa.
Ole ni wetu sisi watoto wa makabwela tusio na baba mbunge wala mama Waziri. Tutazidi kuitwa kwenye Usaili na kulundikwa kama mapipa ya taka tukijipa matumaini ya kupata kazi. Hivi watu 23,000 wanatakiwa 40 na wewe unajihesabia wakati huna hata ndugu yako diwani??
Aliye na "wadhifa" zaidi kwenu ni mjomba wako ambaye amebahatika kupitishwa na CCM kugombea ujumbe wa Kitongoji na hajui kama atashinda. Huyo ndo ukoo mzima unamtegemea, halafu ndo unajipa matumaini ya kuajiriwa TRA?? Ama kweli utakua na wazimu. Na mtoto wa Hawa Ghasia aende wapi? Mtoto wa Makongoro Mahanga aende wapi? Bado mtoto wa dada yake Lukuvi na wa shangazi yake Lusinde. Amka Mtanzania.!
Umetoka kwenu Peramiho umekuja kwenye usaili wa TRA Dar.. huna hata pa kushukia.. Nauli umechangiwa na kijiji maana tangu umalize chuo kikuu hujawahi kufuga hata kuku. Ulipohitimu ulirudi nyumbani ukaendelea kula na kulala kwa wazazi.
Walipokuja kwenye mahafali yako na kusikia umepata "first class" walifurahi na kuamini sasa wanauaga umasikini. Hawakujua kuwa maisha ni zaidi ya "first class" ya darasani.
Uliporudi nyumbani ukaanza kuomba kazi kila ulipoona tangazo la kazi. Lakini hukuwahi kuitwa hata kwenye interview moja.
Umetembea na "bahasha ya kaki" kutembeza CV kwenye maofisi mbalimbali hadi watoto wa mtaani wamekutungia jina "bahasha ya kaki" maana wanakuona nayo kila siku.
Umetembelea mitandao yote ya kazi unayoijua kuanzia "Zoom Tanzania" hadi "Kazi Bongo" lakini hujapata kazi.
Mwaka wa pili sasa huu unaisha bado uko mtaani. Experience ya mtaani imekupa "degree nyingine mbili". Degree ya Maisha magumu na ile ya kutafuta kazi bila mafanikio.
Hatimaye leo umebahatika kuitwa kwenye usaili TRA. Unafurahi na kueleza wazazi. Wanauza ng'ombe uje Dar kufanya usaili. Unakuja kwa matumaini makubwa.. Lakini matumaini hayo yanazimwa unapofika na kukuta umati wa watu mithili ya mashabiki wa mpira wote wakitafuta nafasi hiyohiyo unayoitaka. Mwishowe unajibiwa kuwa "Pole hukufamikiwa kupita kwenye usaili".. Jiulize unarudije kwenu Peramiho??
Nimejaribu kuwaza kuwa ikiwa kila mtu aliyeshiriki usaili wa jana TRA ametumia walau Tsh.200,000/= tu kama gharama ya nauli ya kutoka mkoani pamoja na hela ya kujikimu, basi kwa watu wote 23,653 watakuwa wametumia Tsh.4,730,600,000/=. (Yani Bilioni 4 na milioni 700).
Pesa hizi ni mara 6 ya bajeti ya maendeleo ya wizara ya Afrika Mashariki ambayo ni milioni 800. Pia ni nyingi kuliko pesa walizohongwa Chenge na Prof.Tibaijuka kwa pamoja kupitia Escrow.
Sasa imagine watu wasio na kazi, maisha yamewapiga bado wanaporwa Bil.4 na milioni 700 kwa kisingizio cha kuitwa kwenye "Usaili hewa". Huu ni uhuni.
Lakini cha ajabu wasomi hawahawa wanaodhalilishwa kiasi hiki ndio walio mstari wa nyuma kabisa ktk harakati za mabadiliko. Wengi utawasikia "Sio kila kitu siasa" au "mimi sipendi siasa".. Wanasahau kuwa hali waliyonayo ni matokeo ya mfumo wa siasa wa nchi yao.
Mfumo mbovu wa siasa usiokuwa na vipaumbele vya taifa, usiojali wasomi, usiotengeneza fursa za ajira, usiowezesha wasomi kujiajiri ndio umesababisha vijana hawa kuwa katika hali waliyopo. lakini ukiwaambia wachukue hatua watakuambia "mimi sipendi siasa".
Sasa nikuambie hivi kijana mwenzangu, wewe endelea kutokuipenda siasa uzidi kuchakaa, lakini siasa inakupenda sana. Human Being are political animal by nature. Huwezi kutenganisha siasa na maisha ya mwanadamu unless uwe maiti.
Siasa ndiyo inaamua mfumo wa maisha ya jamii yoyote. umaskini tulionao ni matokeo ya siasa tuliyochagua.. utajiri walionao Marekani, Ujerumani na kwingineko ni matokeo ya mfumo wa siasa yao. So huwezi kusema huipendi siasa halafu ukategemea mabadiiko ya kimfumo. yaletwe na nani??
Ni aibu kijana "graduate" anaomba vocha ya 500; wengine wanakutumia "Tafadhali niongezee salio" wengine ni ulisoma nao chuoni wanakutext "kaka nitumie hata buku 5 sijala mchana" halafu haohao ndio wa kwanza kusema hawapendi siasa.
Wanasahau kwamba kilichowafanya wakose hata vocha ya 500 kwenye simu na kuishia kuomba ni mfumo mbovu wa siasa ya nchi yao.
Wito wangu kwa vijana wasomi ni huu.. Mabadiliko ya kweli yanaanza na wewe. Hakuna awezaye kuleta mabadiliko uyatakayo isipokuwa wewe. Tanzania uitakayo inaanza na wewe.
Wewe kama msomi, toa elimu ya uraia, pinga mfumo kandamizi uliopo, shiriki kikamilifu kwenye chaguzi mbalimbali na chagua viongozi wanaofaa..
Vijana wengi "wasomi" wanapuuza sana kupiga kura.. Ni muhimu kuelewa kuwa ikiwa hutapiga kura utawapa nafasi "wajinga" wakufanyie maamuzi.
Kwa ujumla ni kuwa mfumo wa uongozi wa serikali hii ya CCM umeshindwa kabisa kuleta maendeleo yaliyotegemewa. Mfumo huu umeshindwa kumsaidia kijana msomi kwa kutengeneza fursa za ajira na kumuwezesha kujiajiri.
Ni mfumo uliotabiriwa na Yesu Kristo miaka 2000 iliyopita kuwa "mwenye nacho atongezewa na asiye nacho atanyang'anywa hata kile kidogo alicho nacho".. Ni mfumo kandamizi, ni mfumo usiojali utu.
Shime vijana wenzangu tuwe chachu ya mabadiliko ya nchi yetu hii. Natoa rai tuanze na uchaguzi wa serikali za mitaa kesho then tumalizie na uchaguzi mkuu mwakani. Fanya maamuzi sahihi ambayo hutakuja kuyajutia. Vijana wasomi tusipokua chachu ya mabadiliko tusimlaumu yeyote.
JIPU LIMEPASUKA; SIWEZI KUWA ADUI KWA KUSEMA UKWELI.
Malisa GJ || Your Partner in Critical Thinking.!

0 comments :

Post a Comment

 

Copyright © 2013. THE WORLD OF TODAY - Haki zote zimehifadhiwa
Template Modify by World of Today TEAM
Proudly powered by Blogger