Dar es Salaam. Mwenyekiti mweza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Dk Emmanuel Makaidi amejitolea kusuluhisha mgogoro baina ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na chama chake cha Chadema.
Hatua ya mwanasiasa hiyo mkongwe ambaye pia ni Mwenyekiti wa NLD, imekuja siku chache baada ya kuibuka hoja mbalimbali katika mitandao ya kijamii zikishawishi Zitto kurejea Chadema hasa baada ya kauli yake bungeni kuwa amekuwa akiwakosa wanasiasa wenzake wa upinzani wanaounda kundi la Ukawa.
Ijumaa wiki iliyopita, Zitto alikaririwa na gazeti hili akisema yuko tayari kurudi Chadema kwa sharti kwamba mgororo baina yao ujadiliwe kwa uwazi na upande wenye makosa uombe radhi kwa uwazi pia, huku Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema suala hilo lina njia zake na siyo la kuzungumza katika vyombo vya habari.
Zitto aliingia katika mgogoro na Chadema akituhumiwa kwa mambo mbalimbali ya usaliti na kushiriki mkakati wa kumpindua Mbowe hatua ambayo licha ya kuikana, alivuliwa nyadhifa zake zote ndani ya chama na kuamua kukimbilia mahakamani kunusuru uanachama wake.
Akizungumza katika ofisi za gazeti hili, Dk Makaidi alisema anaamini Zitto amekuwa na nia ya dhati ya kurudi Chadema tangu Machi wakati wa Bunge la Katiba. Alisema Zitto alimfuata na kumweleza nia yake ya kurudi Chadema na kumwomba ampatanishe na Mbowe.
Alisema hatukutekeleza ombi hilo wakati ule kwani alijipa nafasi ya kuona namna atakavyomweleza Mbowe.
Alisema baada ya kuchunguza, aliona Mbowe ni mtu muungwana anayeingilika na wakati analifanyia kazi suala hilo, ndipo alipoona kwenye gazeti hili nia ya Zitto kutaka kurudi Chadema kwa sharti moja.
Hata hivyo, alimshauri Zitto kusimamia nia yake hiyo ya kupatanishwa lakini bila ya kuweka sharti lolote ili kazi ya upatanishi iwe rahisi.
Dk Makaidi alisema jitihada zozote atakazozifanya Zitto nje ya Chadema hazitazaa matunda kwa kuwa ndicho chama pekee kitakachoweza kumsaidia kuendeleza siasa za kuiondoa CCM madarakani bila ya kikwazo.
Hata hivyo, Zitto alipoulizwa kuhusu madai ya Dk Makaidi, alisema hajawahi kuongea naye suala lolote linalohusu kupatanishwa na Mbowe.
“Huyu mzee ni mtu ninayemheshimu sana na juhudi zake ni nzuri, lakini sijawahi kuzungumza naye kuhusu kupatanishwa na chama changu, sisi wenyewe tuna uwezo wa kukaa wawili na kuyamaliza, jitihada zake kwa sasa hazijahitajika,” alisema. Aliongeza: “Ninaamini kwamba umoja wa upinzani ndiyo njia sahihi ya kuweka ushindani wa kisiasa. Ninaamini kwamba vyama mbalimbali vyaweza kuwa katika umoja wa Ukawa. Nisilazimishwe kuwa Ukawa kupitia chama hicho. Naweza kuwa Ukawa kupitia chama kingine chochote ikiwamo CUF, NCCR-Mageuzi au hata ACT- Tanzania. mwananchi
0 comments :
Post a Comment