Utata aliyeghushi saini ya Nyerere, soma hapa upate ukweli wa jambo hili
TAKRIBAN wiki mbili tangu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta kunukuliwa akikiri kughushiwa kwa saini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na iliyopachikwa katika Sheria ya Makubaliano ya Hati ya Muungano kama ilivyo kwa saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa, si Ikulu wala mamlaka nyingine zenye uhakika nani hasa amehusika na kughushiwa kwa saini hizo.
Saini zilizoghushiwa zimo katika hati ya sheria hiyo Namba 22 ya mwaka 1964, iliyosainiwa Aprili 25, mwaka huo wa 1964 na Mwalimu Nyerere kwa nafasi yake ya Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na Msekwa kwa nafasi yake ya Katibu wa Bunge la Tanganyika.
Katika kughushi saini hiyo ya Nyerere, wahusika wameongeza herufi “us” ikiaminika kwamba walifanya hivyo kwa kutumia utaalamu wa kompyuta na katika sehemu ya saini ya Msekwa kuliandikwa neno “Msekwa” kwa njia hiyo hiyo ya kompyuta.
Kwa mujibu wa wananchi kadhaa waliowasiliana na chumba chetu cha habari kutaka kujua aliyehusika katika kughushi saini ya Mwalimu Nyerere, hasa baada ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kuonyesha hati halisi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa waandishi wa habari Ikulu, jijini Dar es Salaam, Jumatatu wiki hii, hatua dhidi ya wahusika hazina budi kuchukuliwa.
“Tumeona kupitia vyombo vya habari sahihi halisi ya Mwalimu Nyerere iliyokuwapo katika hati halisi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambayo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ameowaonyesha waandishi wa habari Ikulu, sasa nani aliyehusika kughushi sahihi ya awali iliyokuwamo kwenye sheria ya makubaliano ya hati ya Muungano?
Hivi kweli saini ya Mwalimu Nyerere inaghushiwa na kusambazwa kwa wabunge? Tunaomba hatua zichukuliwe,” alisema Erick Haule ambaye alipiga simu chumba chetu cha habari kuhoji suala hilo.
Mbali na Haule, mwananchi mwingine aliyepiga simu chumba chetu cha habari na kutaka ufuatiliaji zaidi wa suala hili ni Mwalimu Rehema Mlay, aliyeweka bayana kusikitishwa kwake na namna Bunge linavyoweza ‘kuchomekewa’ nyaraka zilizoghushiwa na baadhi ya watu aliowaita “wahuni”.
Kutokana na hali hiyo, mwandishi wetu aliwasiliana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue ili kufahamu kama kuna hatua zimekwishakuchukuliwa dhidi ya wahusika.
“Kwa upande wangu bado sijapata hizo nyaraka zenye saini ya Baba wa Taifa iliyoghushiwa. Sijui na wala sijaiona bado, kwa hiyo siwezi kutoa maelezo yenye majumuisho kuhusu hilo,” alisema Sefue.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Uhusiano na Uratibu, Steven Wassira alisema hawezi kujua kwa uhakika nini kilichotokea hadi saini ya Mwalimu Nyerere kughushiwa japokuwa maudhui ya kilichomo kwenye hati yenye sahihi hiyo ni sahihi.
Hata hivyo, Wassira na Sefue walitoa maelezo yanayofanana kuhusu uwezekano wa ‘kuchezewa’ kwa saini hiyo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere. Wote walisema huenda nyaraka zenye saini hiyo ya Nyerere na ile ya Msekwa zilichotwa kutoka kwenye mtandao wa kompyuta na wakati wa kufanya hivyo, saini hizo ndipo zilipowezekana kubadilika.
Wiki takriban mbili zilizopita, Sitta alinukuliwa na gazeti moja la kila siku akizungumzia suala hilo akidai walioongeza maneno hayo ni wafanyakazi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kuona sehemu ya maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini akaweka bayana walifanya makosa.
“Wale vijana walipoona document (nyaraka) haisomeki waliongeza “us” mwisho kwa kompyuta kwenye saini ya Nyerere, ila walifanya makosa maana bora kitu kionekane kufifia hivyo hivyo lakini kibaki na maana yake,” alisema.
Lakini hata hivyo, maelezo hayo ya Sitta hayakuwa yameridhiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Jaji Frederick Werema, ambaye kwa wakati huo alinukuliwa na gazeti hilo akisema hafahamu kama ofisi yake inahusika na kuchezewa kwa saini hizo.
chanzo raia mwema, bofya hapa
0 comments :
Post a Comment