BAADHI ya mali za Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba, zilizopaswa kupigwa mnada ili kulipa deni la takriban shilingi milioni 900 analodaiwa katika Benki ya CRDB zimenusurika kupigwa mnada huo, baada ya mteja kujitokeza kununua mali husika siku ya mwisho ya ulipaji deni hilo benki.
Mali za mbunge huyo zilizopaswa kuuzwa ni Shule ya Sekondari ya Bakili Muluzi pamoja na vifaa vyake mbalimbali. Shule hiyo yenye eneo la ukubwa wa mita za mraba zaidi ya 34,000 ilitumika kumpatia mbunge huyo mkopo huo wa Sh milioni 900 kutoka CRDB mapema mwaka 2009.
Deni hilo pamoja na riba ya asilimia 17, liliongezeka na kufikia Sh bilioni 1.2, huku juhudi za mbunge huyo kuishawishi Serikali kununua shule hiyo kabla ya Jumatatu wiki hii, siku ya mwisho iliyokuwapo kwenye mapatano ya kulipwa kwa deni hilo, zikikwama.
Mke wa Komba, Salome, alithibitisha kupata mnunuzi wa shule na alimweleza mwandishi wetu wa gazeti dada na hili la Raia Tanzania Jumatatu wiki hii kwamba; “Tumepata mtu wa kununua, tunamshukuru Mungu, lakini kwa sasa siwezi kumtaja mteja aliyetukomboa hadi tutakapomaliza suala la mikataba.”
Kwa mujibu wa Salome, mnunuzi huyo alijitokeza siku ya mwisho kabla CRDB haijazichukua shule zao mbili ambazo ni Sekondari ya Bakili Muluzi na Shule ya Msingi ya Coletha, tayari kuzipiga mnada.
Katika maelezo yake hayo, Salome Komba alisema mnunuzi huyo atanunua Shule ya Bakili Muluzi pekee na kuiacha Shule ya Coletha chini ya familia ya Kapteni Komba, huku taarifa ambazo bado hazijathibitishwa hadi tunakwenda mitamboni zikibainisha kwamba inawezekana mnunuzi huyo ni Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kama taasisi au mmoja wa wachungaji wa kanisa hilo.
Mizengwe ya mkopo
Katika sakata hilo, jambo linalotia shaka ni uamuzi wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kujaribu kuingilia kati sakata hilo ili kunusuru shule ya Komba kupigwa mnada.
Pinda alifanya majaribio kadhaa ikiwa ni pamoja na kuiandikia Benki ya CRDB kumpa muda zaidi wa nyongeza Komba kulipa deni lake lakini hata maombi ya Pinda kupewa nafasi, bado Komba alishindwa kulipa deni hilo.
Uamuzi huo wa Pinda unahusishwa na kile kinachotajwa kwamba ni kubebana, na hasa pale ulipoibuliwa ushauri kwamba Serikali inunue shule hiyo huku hali halisi ikijibainisha kwamba Serikali imekuwa ikishindwa hata kuimarisha shule zake, zikiwamo za sekondari za kata, achilia mbali kununua shule hiyo ili tu kumnusuru Komba ambaye ni mtu muhimu katika siasa za uhamasishaji kupitia nyimbo katika Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ilivyokuwa kwa Komba
Kwa mujibu wa nyaraka mbalimbali zilizopatikana kama ambavyo gazeti hili liliandika katika toleo lake lililopita, Komba anayemiliki shule kadhaa jijini Dar es Salaam, ikiwamo hiyo ya Bakili Muluzi, alikuwa akidaiwa na CRDB zaidi ya Sh bilioni moja, ambazo ni deni la msingi pamoja na riba ya asilimia 17 katika miaka mitano anayodaiwa kushindwa kulipa deni hilo.
Katika habari ya gazeti hili wiki iliyopita iliwekwa bayana kwamba, deni la msingi ni Sh milioni 900, lililotolewa katika mikupuo miwili; kwanza Sh milioni 300 na baadaye Sh milioni 600, baada ya maombi ya mkopo aliyoyatuma CRDB mwaka 2007, kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa madarasa, nyumba za wafanyakazi, mabweni, uchimbaji wa visima na ununuzi wa samani kwa ajili ya madarasa ya kidato cha tano na sita katika shule yake hiyo ya Bakili Muluzi.
Marejesho ya mkopo huo uliopaswa kulipwa ndani ya miaka mitano, yalitakiwa kufanyika katika mikupuo 22 na kumalizika Juni 30, 2014.
“Januari 14, 2009, Mbunge huyo alipewa na CRDB mkopo wa jumla ya Sh milioni 900 zilizopaswa kulipwa kwa ‘installments’ (mikupuo) 22 na kukamilika Juni 30, 2014,” alisema mtoa habari wetu ambaye ni wazi jina lake hatuwezi kuliweka gazetini kwa sasa.
Katika makubaliano hayo, mbunge huyo kupitia taasisi isiyo ya kiserikali (NGO) anayoimiliki, alipewa ‘grace period’ (kipindi cha muda wa matazamio) wa miezi sita, lakini hata alipoanza kulipa, malipo yake hayakwenda kama ilivyotarajiwa.
“Dhamana ya mkopo huo iliyowekwa benki ni hati tatu za viwanja anavyovimiliki namba 121244 (Plot No, 167/1 Block 1), namba 121245 (Plot No 167/2 Block 1 na namba 55920 (Plot No 1030) vyote vipo Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam,” alisema mtoa habari wetu huku nyaraka kadhaa zikithibitisha.
Vile vile gazeti hili lilibaini kuwapo kwa jitihada za dhati za Mbunge huyo kulilipa deni lake hilo, lakini hadi Aprili 16, mwaka jana, alikuwa amelipa malimbikizo ya deni ya Sh 214,126,678 ambapo Sh 146,126,678 zililipwa katika Akaunti ya Benki ya CRDB, Lumumba namba 01J1008525300.
Fedha nyingine kati ya hizo ambazo ni Sh 68,000,000 zililipwa kwa Mbunge huyo na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) katika akaunti yake iliyopo CRDB Tawi la Kijitonyama, jijini Dar es Salaam na kisha yeye mwenyewe akazihamishia Tawi la CRDB Lumumba.
Gazeti hili halikuweza kufahamu mara moja sababu za TACAIDS kumlipa Mbunge huyo kiasi hicho kikubwa cha fedha.
Kutokana na kuchelewa kulipa deni katika mtiririko waliokubaliana, hadi Novemba 2011, miaka miwili tu tangu apewe mkopo huo, deni hilo liliongezeka na kufikia Sh 1,252,110,349.14, kitendo kilichosababisha Benki ya CRDB kutafuta dalali wa Mahakama na kumtaka akamate mali za mbunge huyo na kuzipiga mnada wa hadhara.
Dalali huyo, Bani Investment Limited, alipewa kazi hiyo Februari 8 mwaka jana, lakini kabla ya kufanya hivyo, Mbunge alikimbilia Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kuweka pingamizi, ingawa tayari wanafunzi kadhaa wa shule anazozimiliki walilazimika kuhamia shule nyingine kutokana na kutofahamu mustakabali wao.
“Wakati wa mgogoro kati yake na CRDB, Mbunge huyo alikuwa akihaha kuhamisha umiliki wa shule zake, kiasi cha kufikia makubaliano na kampuni ya IKS Tanzania kuiendesha moja ya shule zake kwa miaka mitano huku ikilipa deni hilo kwa niaba ya Mbunge, lakini suala hilo lilishindikana,” taarifa zaidi zinafafanua.
Baada ya kuona kuwa suala hilo linazidi kuwa gumu kwake, Raia Mwema linafahamu kwamba, Mbunge huyo ambaye ana uhusiano mzuri na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM na Serikali, aliiomba Ofisi ya Waziri Mkuu (PMO) kuingilia kati suala hilo na kumshawishi Mkurugenzi wa CRDB, Dk. Charles Kimei, amuongezee muda wa kulipa deni lake.
Aprili 23, 2012, PMO ilimwandikia barua Dk. Kimei ikimshawishi kuangalia uwezekano wa kumwongezea muda wakati huo Serikali inatafuta namna stahiki ya kumsaidia kwa kuzinunua shule zake, lakini CRDB iliendelea na msimamo wake wa kutoongeza muda zaidi.
Machi 21 mwaka jana, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliijibu barua ya Mbunge huyo ya Februari 20, mwaka huo huo ambayo haikuwa na kumbukumbu namba, ikimtaarifu kuwa pamoja na kupokewa kwa barua hiyo, taarifa zilizokifikia chumba cha habari zilisema kwamba, maombi ya Jiji kununua shule na ardhi anayoimiliki, kwamba yatashughulikiwa na Kamati ya Huduma za Jamii; na hadi sasa hakuna majibu aliyopewa.
Kwa sasa, zikiwa zimesalia siku hizo tano tu kufika Juni 30, 2014 ambayo ni siku ya mwisho wa makubaliano, CRDB imekuwa ikiiomba Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kuiruhusu kuuza mali zote za Mbunge huyo kufidia deni lao, lakini Mbunge anadai kuwa thamani ya shule zake na ardhi ipatayo mita za mraba 34,735, ni zaidi ya deni analodaiwa. chanzo raia mwema
0 comments :
Post a Comment