Pata Habari Motomoto za Nje na Ndani ya Nchi kwa njia ya E-mail, Andika E-mail yako hapo chini.


Home » » Katiba Ilivyopatikana, Soma ucheke

Katiba Ilivyopatikana, Soma ucheke


Katiba Ilivyopatikana
  • Chenge nusura asuse
  • Mawaziri Zanzibar, Bara wakutana mara mbili.

VIONGOZI kutishia kuachia nyadhifa, vikao vya mara kwa mara vya mawaziri wa Muungano na Zanzibar na kupandwa jazba miongoni mwa wajumbe wa Bunge la Katiba ni miongoni mwa masuala yaliyojitokeza wakati wa mchakato wa kutafuta Katiba Pendekezwa unaokamilika leo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana baada ya mahojiano na wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK), taarifa rasmi za Bunge kutoka ndani ya vikao vya kamati hizo na duru za Bunge lenyewe, Raia Mwema limepata picha ya nini hasa kiliendelea nyuma ya pazia.

Miongoni mwa taarifa ambazo gazeti hili limezipata ni hatua ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi wa Katiba, Andrew Chenge, kutishia kuachia ngazi endapo wajumbe wa Kamati hiyo wangelazimisha vitu ambavyo vingeweza kushusha heshima ya Kamati.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi za Kamati, Chenge alitoa maelekezo hayo baada ya baadhi ya wajumbe wa Kamati yake kutaka mfumo wa sasa wa kuwa na rais na mgombea mwenza wake ubadilishwe na badala yake rais awe na makamu wawili ambao ni rais wa Zanzibar na waziri mkuu wa Tanzania.

Chenge alikuwa amependekeza kwamba rais wa Jamhuri ya Muungano anatakiwa kuwa na makamu ambaye ni mgombea mwenza kutoka katika chama chake; huku akiwa na makamu wengine wawili ambao ni rais wa Zanzibar na waziri mkuu wa Tanzania.

“Kama mnataka kuondoa nafasi ya mgombea mwenza na halafu tuwe na rais wa Zanzibar na waziri mkuu basi mtafute mtu mwingine wa kuwasilisha mawazo hayo. Hapo tutakuwa tunafanya kazi ambayo watu watatushangaa.

“Huko mbele ya safari, inaweza ikatokea kuwa rais wa Zanzibar akatoka katika chama tofauti na rais wa Tanzania. Sasa kama hakuna mgombea mwenza na tatizo likimkuta rais, maana yake mrithi wake atakuwa anatoka katika chama tofauti.

“Kwa mujibu wa Katiba ya sasa na hata hii inayopendekezwa, waziri mkuu anatakiwa kutoka katika chama chenye wabunge wengi. Je, ikitokea kwamba waziri mkuu akatoka katika chama tofauti na rais wake; yaani rais akapata kura nyingi kuliko wabunge wake; je, si mtapata rais kutoka chama kingine hapo,” alihoji Chenge.

Taarifa hizo za kwenye maandishi zinathibitishwa na baadhi ya wajumbe waliokuwamo katika Kamati hiyo ambayo, hata hivyo, wanaeleza kwamba busara ilitumika na hatimaye mapendekezo hayo ya Chenge ndiyo ambayo yameingia katika Katiba Pendekezwa.

Katiba hiyo inapendekeza kuwa na makamu watatu wa rais ambao ni mgombea mwenza anayekuwa makamu wa kwanza, rais wa Zanzibar atakuwa makamu wa pili huku waziri mkuu akiwa makamu wa tatu.

Taarifa kutoka ndani ya kamati hiyo zinaeleza kwamba hata hivyo Chenge alikuwa kiongozi asiye na jazba katika kamati yake hiyo na kwamba pengine kazi ingekuwa ngumu endapo Mwenyekiti angekuwa Dk. Asha Rose Migiro ambaye alielezwa kuwa na msimamo mkali.

Raia Mwema limeelezwa pia kwamba wakati BMK likiendela, kulifanyika vikao walau viwili vya mawaziri wa Muungano na wale wa Zanzibar, hususan, wakati wa kujadili masuala ya kifedha ndani ya Katiba mpya.

Ni vikao na majadiliano hayo makali, gazeti hili limeelezwa, ndivyo ambavyo hatimaye vilisababisha kuitwa Dodoma kwa Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndullu, pamoja na wasaidizi wake, ili kueleza masuala ya kifedha na Muungano.

“Unajua watu wanadhani kwa vile bungeni walibaki wabunge kutoka CCM na wale wasio na mrengo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), basi BMK lilipoa. Nakuhakikishia kwamba Bunge lilikuwa active sasa.

“Kuna wakati jazba zilikuwa zinapanda hadi watu mnaamua kuweka mapumziko au kuita wataalamu kutoka nje ili mpate maelezo ya kina. Wale ambao walikuwa nje, wamekosa mambo sana,” alisema mmoja wa wajumbe wa BMK ambaye hata hivyo hakupenda kutajwa jina lake.

Katiba Pendekezwa inatarajiwa kukabidhiwa kwa Marais Jakaya Kikwete na Dk. Ali Mohamed Shein katika tukio lililopangwa kufanyika katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kuanzia saa nane mchana leo.

Tangu juzi usiku, magari maalumu ya matangazo yamekuwa yakipita katika mitaa mbalimbali ya Dodoma kuwahamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi katika tukio hilo linalotarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wote wa juu kitaifa.

Katiba Pendekezwa ni kubwa na yenye mambo mengi kuliko Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba kwa vile yenyewe imejikita katika mfumo wa Serikali Mbili wakati ile ya Tume ilikuwa kwa ajili ya Serikali Tatu.

Ina Ibara 18 zaidi ya ile ya Tume; ina jumla ya Ibara 289 kulinganisha na 271 za Rasimu.

Wakati akiwasilisha Katiba Pendekezwa bungeni, Chenge, alisema Katiba imechukua Ibara 233 kutoka katika Rasimu ya Tume ya Katiba.

Alisema kati ya hizo, ibara 47 zimebaki kama zilivyo pasipo kufanyiwa marekebisho yoyote, huku 186 zikiwa zimefanyiwa marekebisho, 28 zimefutwa na Ibara 41 ni mpya zikiwa zimetokana na mapendekezo ya BMK.

Mwaliko wa shughuli hiyo unawagusa wabunge wote wa Bunge la Tanzania, wakiwamo wale wa UKAWA, Raia Mwema linafahamu kuwa wabunge wameagizwa kuwa Dodoma kuanzia jana.

Kutokana na rasimu ya ratiba ya makabidhiano hayo ya leo ambayo gazeti hili limeona nakala yake, Kikwete atakuwa mzungumzaji mkuu katika tukio hilo, ingawa Mwenyekiti wa BMK Samuel Sitta pia atapewa fursa ya kuzungumza.

Ratiba inaonyesha pia kuwa kutakuwa na neno la shukrani kutoka kwa makundi yote matatu makuu ambayo yaliunda BMK. Hayo ni ya wajumbe kutoka Baraza la Wawakilishi, wajumbe kutoka Bunge la Tanzania na wajumbe 201 kutoka makundi mbalimbali ambao waliteuliwa na Kikwete kuingia katika BMK.

Viongozi wengine wa kitaifa wanaotarajiwa kuhudhuria shughuli hiyo ni Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Spika wa Bunge, Anna Makinda; Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho na Jaji Mkuu wa Tanzania, Chande Othman. RAIA MWEMA

0 comments :

Post a Comment

 

Copyright © 2013. THE WORLD OF TODAY - Haki zote zimehifadhiwa
Template Modify by World of Today TEAM
Proudly powered by Blogger