Dar es Salaam. Vyama vya CUF na Chadema vimekitupia lawama Chama cha Mapinduzi (CCM) vikidai kimecheza rafu katika mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika leo.
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti viongozi wa
vyama hivyo walidai kuwa CCM imekuwa ikicheza mchezo mchafu kwa
kuwarubuni na kuwanunua wagombea wake maeneo mbalimbali nchini.
Tangu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi huo mapema
mwezi huu, CCM imekuwa ikitupiwa lawama za kuhujumu wapinzani na kwamba
inatumia nafasi iliyonayo ya chama tawala kuvikandamiza vyama pinzani.
Hata hivyo, alipotafutwa Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye ili kujibu shutuma hizo zilizotolewa na vyama
vya Chadema na CUF alisema: “Siwezi kujibu chochote kwa sababu nyie
ninapotoa majibu yangu hamuandiki ipasavyo lakini hao... Mnawaweka
kipaumbele. Sasa basi andika walichosema halafu mimi kesho (leo)
nitawajibu walichokisema kama kitakuwa na maana.”
Awali, huku akijigamba kuwa na asilimia 85 ya
wagombea katika nafasi mbalimbali za uongozi, Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema: “Lakini yapo maeneo ambayo
dakika za mwisho wagombea wetu ama kwa makusudi ama kwa bahati mbaya
wakaingia mitini.”
“Asilimia nyingine zimekuja kupungua kwa hila na
njama ambazo zimekuwa zikifanywa na CCM, zikiwamo kununua wagombea wetu,
kuwateka, kuwanyanyasa kisaikilojia na maeneo mengine machache ni
kutokana na mapingamizi yaliyowekwa ambayo hayakuwa na mantiki,”
alieleza Mwalimu.
Kwa upande wake, Kaimu Naibu Katibu Mkuu na
Mkurugenzi wa Mpango na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alidai kuwa wana
uthibisho wa kutosha kwamba CCM kwa kutumia mikono ya Serikali
wamejiandaa kuvuruga zoezi la uchaguzi huo ili kupora ushindi,
unaoelekea kwenye vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“CCM wameandaa karatasi za kupigia kura zenye
alama ya vema kwa mgombea wao ambazo watawapa wananchi waiingie nazo
kwenye chumba cha kupiga kura na kuwalipa kati ya Sh5,000 hadi Sh10,000
kwa atakayefanikisha mpango huo,” alisema Mketo huku akiwaonyesha
waandishi wa habari mfano wa karatasi hizo na kuongeza:
“Walianza mbinu hizi kwa kuwaengua wagombea wetu
ili wa kwao wapite bila kupingwa katika maeneo ambayo Ukawa wana nguvu
ila kwa hili la karatasi, tutapambana hadi mwisho.”
Akizungumzia juu ya mwitikio wa kujiandikisha
katika zeozi la leo la kupiga kura, Mwalimu alisema kuwa Dar es Salaam
imekuwa na mwitikio hafifu kulinganisha na mikoa mingine nchini.
“Mimi nashangaa sana, badala ya watu wa jiji hili
kujitokeza kujiandikisha ili waweze kupiga kura na hatimaye wapate
viongozi wanaowataka kushughulikia matatizo yao wao wanagoma…Ni asilimia
43 tu ya wakazi wa jiji hili waliojiandikisha kupiga kura leo,” alisema
Mwalimu kwa masikitiko.
Alisema watu wengi hawana mwitikio kwa madai kuwa
wanashughuli nyingi na wengine wakidai kuwa Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa unawagusa watu wa vijijini ambako kuna matatizo mengi.
0 comments :
Post a Comment