Serikali ya awamu ya nne kumaliza vibaya’
Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Awamu ya Nne imebakiza takriban mwaka mmoja kuondoka madarakani, sifa ya Tanzania kwenye jumuiya ya kimataifa imeendelea kutiwa doa kutokana na kuhusishwa na ongezeko la ufisadi wa mabilioni ya fedha za umma na ujangili.Kutokana na hali hiyo, huenda uongozi wa awamu hiyo iliyo chini ya Rais Jakaya Kikwete ikaiacha nchi vibaya na historia ya pekee ya kuwapo kwa ‘mikwaruzano’ kati yake na wafadhili mbalimbali wanaoelezwa kutoridhishwa na namna fedha za umma zinavyochotwa na wajanja wachache wakiwamo viongozi wa umma.
Alipotafutwa kuzungumzia hali hiyo na hatua ya wafadhili kusitisha misaada yake kwa Serikali inayoisimamia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Kwanza sina taarifa za kutosha kuhusu msimamo wa Marekani na suala zima la MCC na escrow zaidi ya kuziona kwenye magazeti yenu.”
Aliongeza: “Kwa kuwa sina taarifa rasmi, siwezi kusema chochote kuhusu hilo.”
Juzi, Balozi wa Marekani nchini, Mark Childressi alieleza kuwa nchi yake haitatoa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Milenia (MMC) kwa Serikali ya Tanzania, hadi itekeleze maagizo ya Bunge kuhusu uchotwaji wa fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow. Kauli ya kiongozi huyo imedhihirisha ukubwa wa tatizo hilo, ingawa Ikulu imeshasema haitekelezi maagizo kwa shinikizo la misaada.
Katika tamko lake kwa umma, balozi Childress alisema: “Kupigwa hatua katika mapambano dhidi ya rushwa ni muhimu sana kwa mkataba mpya kati ya MCC na Tanzania na katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara Tanzania.”
Aliongeza: “Tunatoa wito kwa Serikali kuchukua hatua za haraka kuhusu suala hili hasa kutokana na uzito wake katika masuala muhimu kadhaa ya maendeleo.”
Uamuzi huo umekuja wiki kadhaa baada ya wafadhili katika nchi mbalimbali nao kuzuia kiasi kikubwa cha fedha kutokana na sakata la uchotaji wa fedha za escrow Sh306 bilioni kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Hata hivyo, Waziri wa Fedha Saada Mkuya akizungumzia taarifa hizo hivi karibuni, alisema hakuna mfadhili aliyekataa kutoa fedha, bali mazungumzo yalikuwa yakiendelea vizuri.
“Nataka kuwahakikishia kwamba washirika wetu wa maendeleo ambao wanatoa fedha kwa mfumo kusaidia bajeti kuu ya Serikali, hawajasitisha msaada.
Kulikuwa kuna majadiliano baada ya kuonyesha wasiwasi...Walikuwa wakisubiri Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili waweze kutoa. Fedha hizo ni Sh922 bilioni na hapa tunapozungumza Finland na Idara ya Maendeleo ya Kitaifa (DFID) wameshatoa kiasi chao,” alisisitiza.
Hata hivyo, wakati Serikali ikisema hayo, Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira (EIA) wameitaka MCC kutokubali kuidhinisha mkabata huo na Tanzania wa Dola 450 milioni za Marekani (Sh700 bilioni), hadi Rais Kikwete atakapochukua hatua stahiki dhidi ya rushwa iliyotawala na sakata la ujangili na usafirishwaji wa pembe za ndovu kwenda nje hasa China.
Taasisi hiyo inayojihusisha na masuala ya mazingira, ilitoa wito huo jana kwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry na Mwenyekiti ambaye pia ni Mkurugenzi wa MCC, Diana Hyde kwamba wasitishe hatua hiyo kwa Tanzania. mwananchi
0 comments :
Post a Comment