Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
Waziri Mkuu
mstaafu, ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, ameiomba
serikali kutokandamiza haki za msingi za raia na kujali haki za
wanyamapori. Hata hivyo, amewataka raia kuheshimu mipaka.Akizungumza katika mkutano wa kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa na vitongoji Bwawani, Mto wa Mbu, wilayani Monduli, Lowassa alisema pamoja na matatizo yaliyoko, ni muhimu haki za raia zikalindwa.
“Hapa Bwawani najua mna matatizo na Bational Park (Hifadhi ya Taifa)...naomba Serikali isifanye haki za wanyamapori kwa kugandamiza haki za msingi za raia,” alisema Lowassa.
Aliongeza: “Tunaheshimu sana utalii kwa sababu unatuingizia fedha, lakini tuheshimu haki za msingi za raia..na nyinyi tuheshimu mipaka iliyowekwa.”
Eneo hilo limekuwa na mgogoro na Hifadhi ya Taifa ya Manyara inayopakana nayo, suala ambalo ni moja ya kero kubwa kwa wakazi wake.
Akizungumzia wana-CCM waliyojitoa chama hicho, Lowassa alisema: “Anayetupinga, atupinge kwa hoja..Kama kero hazijatatuliwa...siyo unaamua kutoka halafu unataka uhongwe ili urudi.”
Aliongeza kuwa ndani ya chama wanagombania utekelezaji wa Ilani na hapo ni haki kwa mwanachama kukasirika iwapo Ilani haitekelezwi, lakini si vinginevyo.
Mapema, akizungumza katika mkutano wa kampeni kwenye kijiji cha Migombani, Kata ya Majengo, Lowassa ambaye anatajwa kutowania tena ubunge na kuelekeza nguvu kwenye urais, alijinasibu kwa mafanikio aliyoyapata katika kipindi chake cha miaka 20 ya ubunge.
“Mwaka 1995 wakati naingia ubunge, mtu ukija hapa Mto wa Mbu lazima ulale, huwezi kutoka Monduli kuja hapa na kurudi...barabara ilikuwa mbaya kabisa,” alisema na kuongeza anajivuna kuwa wamemaliza utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya chama.
Alisema serikali ya awamu ya nne imefanya makubwa, ikiwa ni pamoja na usambazaji umeme na maji vijijini.
0 comments :
Post a Comment