David Kafulila
MBUNGE wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila (NCCR-Mageuzi), jana alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Kigoma akituhumiwa kwa makosa mbalimbali aliyoyafanya katika mkutano wa hadhara.
Mkutano huo ulifanyika hivi karibuni katika Kata ya Nguruka iliyopo Wilaya ya Uvinza, mkoani humo ambapo jeshi hilo linadai Bw.Kafulila aliikashifu Serikali na kuchochea mgomo kwa wananchi wasishiriki kuchangia ujenzi wa maabara jimboni humo.
Akizungumza na Majira kwa njia ya simu baada ya kuachiwa kwa dhamana kituoni hapo, Bw. Kafulila alikiri kukamatwa na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi.
Alisema alikwenda kituoni hapo kwa lengo la kuwawekea dhamana wagombea wa chama hicho ambao walikuwa wakishikiliwa na polisi kwa kosa la kutumia vibaya fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Aliongeza kuwa, baada ya kufika kituoni hapo, alikamatwa na polisi wa kituo hicho, kuanza kuhojiwa na kufunguliwa mashtaka matano lakini shtaka la uchochezi kwa wananchi ili wasishiriki kuchangia ujenzi wa maabara halikuwepo kama ilivyodaiwa na jeshi la polisi.
“Miongoni mwa mashtaka niliyofunguliwa ni kumtuhumu Rais Jakaya Kikwete na kuzungumzia ugonjwa wake, shtaka la pili ni kudai Mkuu wa Wilaya ya Uvinza alipewa nafasi hiyo wakati ana kesi ya ufisadi wa mbolea Wilaya ya Chato na Mkurugenzi wa Uvinza amepewa cheo hicho wakati ana kashfa ya rushwa Kondoa,
“Mashtaka mengine ni polisi kupewa mshahara wa sh.300,000 na bunduki lakini kwa kuwa mshahara huo ni mdogo, wanaenda kusumbua watu,” alisema Bw. Kagulila.
Aliongeza kuwa, shtaka jingine ni kuwaambia wananchi wa Kitongoji cha Ruhama, Kijiji cha Bweru wapo kihalali katika eneo hilo hivyo agizo la Mkuu wa Wilaya kuwataka watoke lipo kinyume cha sheria na akienda kuwavamie wampige kwa sababu ni mchochezi.
Bw.Kafulila alisema Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Wilaya ndie aliyemuwekea dhamana saa 12 jioni na ataendelea kuwa mkoani humo kwa ziara za kuwatambulisha wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti katika jimbo lake na kuzungumzia miradi mbalimbali aliyoitekeleza jimboni.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Jafari Mohamed, alipohojiwa kuhusu suala hilo alisema baada ya upelelezi kukamilika watatoa taarifa rasmi. credit majira
0 comments :
Post a Comment