mhe Zitto Kabwe
soma makala ya ZITTO KABWE KUHUSIANA NA SAKATA LA ESCROW
Unyenyekevu ( kuwa na kiasi )
Mwaka 2007 Agosti 14, nilisimamishwa Kuhudhuria vikao vya Bunge kwa kosa
la kumwita Waziri wa Nishati na Madini Bwana Nazir Karamagi muongo.
Kiukweli nilisimamishwa kwa sababu nilitoa hoja Bungeni iliyoiabisha
Serikali - Hoja ya Buzwagi. Wananchi walikasirishwa na kitendo hicho na
kuamua kunipokea kwa maandamano makubwa sana nilipoingia Jijini Dar Es
Salaam na kwenye mikoa mingine niliyofanya ziara. Mawaziri waliotumwa
kueleza maamuzi ya Bunge walizomewa na kumwagiwa mchanga. Mzee Samwel
Sitta, Spika wa Bunge la Tisa, alikuwa anatumiwa sms za 'kifedhuli' kwa
mujibu wa maneno yake; nyingine alinitumia kunisihi nizungumze na '
wafuasi' wangu ili waache kufanya hivyo. Hasira ya Wananchi ilikuwa
kubwa sana na ilionekana wazi wazi.
Siku ya tarehe 19 Agosti nilitoka Dodoma kuelekea Dar Es Salaam. Kabla
sijafika Chalinze ya Dodoma alinipigia simu kaka yangu Abdurahman
Mbamba, akanisihi sana kuwa mnyenyekevu kwa maongezi yangu. Nasaha hizi
kwa kweli zinaniongoza mpaka leo hii. Kwenye mafanikio ya jambo fulani
au hata kutofanikiwa, nakumbuka maneno ya Abdurahman Mbamba.
Nilipokuwa nahutubia Jangwani siku hiyo, niliongea kwa ufupi sana. Watu
wakapiga kelele niendelee kuongea. Ningeweza kuongea nitakavyo maana
ndio nilikuwa ' star' wa nyakati. Mshale wa nasaha zile ukanichoma '
kuwa mnyenyekevu '! Nikawaambia wananchi ' siwezi kuendelea kuongea,
nina Viongozi wangu hapa'. Alikuwapo Mheshimiwa Freeman Mbowe, Dkt.
Willibrod Slaa, Mheshimiwa Augustine Mrema, Maalim Seif Sharif Hamad,
ndg. Ibrahim Lipumba na Bwana James Mbatia. Kwa unyenyekevu nilishuka
jukwaani na kutoa nafasi kwa Viongozi kuzungumza. Watu walitaka na
ningetaka ningeendelea lakini la hasha, nilikataa.
Rais aliunda Kamati ya kupitia Mikataba ya Madini. Aliniteua katika
Kamati ile iliyoongozwa na Jaji Mark Bomani. Watu wangu wengi ' wa
karibu' walinisihi nisikubali kuingia kwenye kamati. Mmoja alithubutu
kuniambia ' snubb him' akimaanisha Rais. Kwamba ningepata umaarufu
zaidi. Ningeweza kukataa na kuwafurahisha watu waliotaka kumwaibisha
Rais. ' kuwa mnyenyekevu' yakawa ni maneno yananirudia kila wakati. Hilo
na kiu ya kuijua Sekta ya Madini vilivyo yalinishawishi kukubali uteuzi
ule. Walionishawishi kukataa hawakunisamehe mpaka leo. Utawasikia
wakisema ' Kamati ya Bomani haikufanya lolote'. Wakati huo huo wanakuwa
mstari wa mbele kufurahia mabadiliko makubwa sana kwenye Sekta ya Madini
ikiwemo kuongezeka Mapato ya kikodi, umiliki wa Serikali kwenye migodi,
Madini ya Vito kuchimbwa na Watanzania pekee na hata kuanza kutozwa kwa
Kodi ya ongezeko la mtaji ( capital gains tax ). Yote hayo yametokana
na mapendekezo ya Kamati ya Bomani yaliyozaa Sera mpya ya Madini ya
mwaka 2009 iliyopelekea Sheria mpya ya Madini ya mwaka 2010.
Mwaka 2014 tunaufunga kwa suala la akaunti ya Tegeta Escrow. Bunge
lilifanikiwa kupitisha maazimio 8 yaliyowasilishwa Serikalini kwa
utekelezaji. Maazimio hayo yalipatikana kwa maridhiano ya Bunge zima. Ni
mafanikio makubwa ambayo yanashawishi wahusika wakuu kufurahia au hata
ku 'claim credit'. Mbunge mmoja kijana rafiki yangu kutoka Mkoa wa
Arusha akaniambia ' brother this is your resurrection ' na usiache.
Mwandishi mmoja wa gazeti la kila wiki akaniambia ' it's a come back '
na kunitaka nifanye ziara Nchi nzima kuelezea suala hili. Wenzangu
kwenye Siasa wakaandaa maandamano Jijini Dar ambayo nilikataa. Shemeji
yangu mmoja akaniambia ' kwenye ushindi jua pa kuishia'. Maneno haya
hayana tofauti na nasaha za Abdurahman.
Sasa kuna juhudi kubwa za kutetea waliotajwa na Taarifa ya Kamati ya
PAC. Magazeti, haswa ya Serikali yamekuwa yakiandika habari zenye
mwelekeo wa kutetea. Ikulu imeagiza Taarifa ya CAG ichapwe kwenye
magazeti, jambo ambalo halijapata kutokea huko nyuma kwani sio mara ya
kwanza PAC kutumia Taarifa ya CAG kuwajibishana. Makala zinaandikwa
kumshawishi Rais asitekeleze maamuzi ya Bunge. Nasaha za ' know where to
stop ' na ' kuwa mnyenyekevu ' zinanivuta na kunishawishi kutosema
lolote.
Hekima inataka kumwachia Mkuu wa Nchi kuamua kwa namna itakavyompendeza.
Tumwache aamue. Unyenyekevu unataka hivyo. Wenye ushawishi tofauti
walikuwa na nafasi Bungeni. Walishindwa ndani ya Baraza la Taifa.
Unyenyekevu ni kwa walioshindwa pia. mwananchi
0 comments :
Post a Comment