Pata Habari Motomoto za Nje na Ndani ya Nchi kwa njia ya E-mail, Andika E-mail yako hapo chini.


Home » » mwanzo Habari Kitaifa Kitaifa Marekani yacharuka escrow;Tanzania yakosa mabilioni ya MCC, ni Dola 450 milioni

mwanzo Habari Kitaifa Kitaifa Marekani yacharuka escrow;Tanzania yakosa mabilioni ya MCC, ni Dola 450 milioni



Dar es Salaam. Wakati Serikali ya Marekani ikisema haitatoa fedha za Changamoto za Milenia (MCC) hadi utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu ufisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow wa Sh306 bilioni utakapofanyiwa kazi, Ikulu imesema, Rais Jakaya Kikwete hatatekeleza agizo hilo kwa shinikizo la msaada huo.


MCC ni taasisi ya Serikali ya Marekani inayotoa misaada kwa nchi zinazoendelea. Shughuli za MCC zinajengwa katika msingi kwamba msaada utaleta ufanisi na matokeo makubwa zaidi pale tu unapoimarisha utawala bora, uhuru wa kiuchumi na uwekezaji katika watu ambao unakuza uchumi na kuondoa umaskini.


Taarifa hiyo ilisema Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la MCC kupitia taarifa yake kwa umma iliyotolewa jana na Ubalozi wa Marekani nchini ilisema, katika mkutano wa bodi hiyo uliokutana Desemba 10 mwaka huu nchini Marekani, ulielezea hofu na masikitiko kuhusu hali ya rushwa inavyoendelea Tanzania.


Fedha ambazo Tanzania ilipaswa kupata kupitia mradi huo wa MCC awamu ya pili ni Dola 450 milioni ambazo ni sawa na Sh765 bilioni.


“Japokuwa bodi ilipiga kura ya kuiruhusu Tanzania iendelee na maandalizi kwa ajili ya mkataba wa pili kwa dhati kabisa, inaihimiza serikali ya Tanzania kuchukua hatua thabiti na mahsusi za kukabiliana na rushwa kama sharti la msingi kwa bodi hiyo kufanya uamuzi wa mwisho wa kuidhinisha mkataba huo.


“Bodi ilieleza kutambua umuhimu wa kusubiri na kuona utekelezaji kamilifu wa tamko lililotolewa na Ikulu ya Tanzania hapo Desemba 9 mwaka huu kwamba itachukua hatua za haraka na kutoa uamuzi dhahiri na thabiti kuhusu maazimio ya Bunge juu la suala la IPTL,” ilieleza taarifa hiyo.


Katika tamko hilo kwa umma, Balozi wa Marekani nchini, Mark Childress alisema “Kupigwa hatua katika mapambano dhidi ya rushwa ni muhimu sana kwa mkataba mpya kati ya MCC na Tanzania na katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara Tanzania.”


Aliongeza: “Tunatoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuhusu suala hili hasa kutokana na uzito wake katika masuala muhimu kadhaa ya maendeleo,” ilisema taarifa hiyo.


Hali kadhalika, Bodi iligusia makubaliano kadhaa yaliyofanyika na Tanzania iliahidi kufanya mageuzi ya kisera, kimuundo na kitaasisi ili kuongeza ufanisi na uwazi katika taasisi zake na katika sekta ya nishati.


Balozi Childress aliendelea kusema, “Tunafurahi kwamba mchakato wa majadiliano ya maandalizi ya mkataba wa pili utaendelea kwa miezi kadhaa ijayo. Tunapenda kusisitiza kuwa ni lazima ahadi hizi zitekelezwe kabla Marekani haijafanya uamuzi wa mwisho kuhusu mkataba wowote mpya na Tanzania.”


Katika mkutano huo, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 10 zilizojadiliwa na Bodi ya MCC iliyokutana kuangalia kama nchi hizi zimekidhi vigezo vya kuendelea na mchakato wa kuandaa mikataba mipya.


Iwapo mkataba huo utapitishwa, utakuwa wa pili wa MCC kwa Tanzania kati ya mwaka 2008 na 2013 ambao ulitekeleza mkataba wa uwekezaji wenye thamani ya Dola za milioni 698 sawa na Sh1.18 trilioni ambao uliowezesha utekelezaji wa miradi ya maji, barabara na nishati ya umeme nchini kote Tanzania. mwananchi

0 comments :

Post a Comment

 

Copyright © 2013. THE WORLD OF TODAY - Haki zote zimehifadhiwa
Template Modify by World of Today TEAM
Proudly powered by Blogger