MFANYABIASHARA maarufu nchini, Reginald Mengi, inadaiwa, ni kati ya watu wanaotishwa kutokana na sakata la fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, lililomalizika bungeni wiki iliyopita.
Alipotafutwa wiki hii, kuhusiana na madai hayo ya vitisho, Mengi, katika mazungumzo ya simu na Raia Mwema, alisema kwa kifupi: “Mimi nimemwachia Mungu masuala yote ya usalama na uhai wangu”.
Mengi anaelezwa kuwa hatarini kwa maelezo kwamba alifadhili wabunge waliokuwa wakishinikiza kung’olewa kwa watendaji wa Serikali na wanasiasa, wanaotajwa kuhusika na kashfa hiyo.
“Mengi ana mawili. Moja anadaiwa kuwafadhili akina Sendeka (Christopher ole) ili wawe mwiba kwa Serikali. Pili, vyombo vyake vya elektroniki vilikuwa vikiripoti sana mambo hayo. Sasa haya ni mambo yanayomkabili,” kilisema chanzo cha gazeti hili.
Wengine, pamoja na Mengi, ambao kwa nyakati tofauti wameliambia Raia Mwema kuwa nao wanatishwa ni pamoja na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila; Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe; Mbunge wa Simanjiro, ole Sendeka na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono.
Wanasiasa na wafanyabiashara hao wanadaiwa sasa kuwindwa na watu ambao wanaelezwa kutofurahishwa na namna walivyosababisha suala hilo kudakwa na vyombo vya habari na umma kiasi cha kuiweka Serikali katika wakati mgumu.
Wakati Kafulila tayari ametoa taarifa katika Jeshi la Polisi kuhusu kutishiwa maisha, Mkono amedai kulishwa sumu wakati akiwa katika ziara ya kibunge nchini Uingereza mwezi uliopita.
Ole Sendeka, mmoja wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayefahamka kuwa na tofauti kubwa na uongozi wa Wizara ya Nishati na Madini wa Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi, na ambaye yuko karibu sana na Mengi, amedaiwa pia kuwekwa kwenye orodha ya watu walio hatarini.
Alipohojiwa na gazeti hili kuhusu vitisho anavyopokea kutokana na msimamo wake kwenye sakata la escrow, Kafulila alisema yeye alianza kutishiwa maisha tangu alipoanza kupigia kelele suala la mabilioni ya escrow mwanzoni mwa mwaka huu na kwamba hata maisha yake yamebadilika.
Wakati wa Mkutano wa Bunge uliomalizika mjini Dodoma wiki iliyopita, Kafulila anasema alikwenda kushitaki Jeshi la Polisi kutokana na meseji za kutisha alizokuwa akitumiwa kupitia simu yake ya mkononi na watu wasiofahamika.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili juzi Jumatatu jioni, Zitto alikiri kufahamu kuhusu hatari inayowakabili na akasema wakati wa Bunge lililopita, hakuwa akila popote zaidi ya nyumbani kwake ambapo dada yake ndiye aliyekuwa akimpikia.
“Nafahamu ni kwa kiasi gani watu walikuwa wakichukizwa na msimamo uliokuwa ukionyeshwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ((PAC) na baadhi ya wabunge na ndiyo maana sasa wako makini kuliko wakati mwingine wowote ule,” alisema Zitto.
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma tayari limekiri kupokea taarifa za kutishwa kwa baadhi ya wanasiasa hao na limekiri kwamba linachunguza taarifa hizi.
Tayari Polisi mkoani Dodoma inadaiwa kumshikilia mtu mmoja ambaye hajatajwa jina kwa madai kwamba alikwenda mkoani humo kuwadhuru baadhi ya wabunge.
Taarifa za vitisho dhidi ya Mengi na wanasiasa hao zinaibua hofu kwamba huenda makundi yenye mrengo wa kimafia yameanza kujitanua hapa nchini katika siku za karibuni.
Tayari kuna matukio ya waandishi wa habari na wana harakati kuteswa vibaya kwa kung’olewa kucha na unyama mwingine baada ya kuonekana kuingilia maslahi ya makundi fulani ya watu wenye nguvu na ushawishi hapa nchini. bofya hapa kusoma zaid
0 comments :
Post a Comment